Joy FM
Joy FM
12 September 2025, 08:24

Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Mkoani Kigoma imezindua dawati la uwezeshaji biashara ili kusaidia wafanyabiashara wadogo na wakubwa kuinuka kiuchumi huku wakiomba dawati hilo kusaidia kuondoa changamoto ya kubambikizwa kodi.
Na Kadislaus Ezekiel
Mamlaka ya mapato (TRA) Mkoa Kigoma imesema kuwa kuanza kutekeleza majukumu yake kwa dawati la uwezeshaji la mamlaka hiyo kutawezesha kutekelezwa kikamilifu kwa changamoto za wafanyabiashara zinazojitokeza ili kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
Meneja wa TRA Mkoa Kigoma, Beatus Nchota amesema hayo mjini Kigoma wakati wa uzinduzi wa dawati hilo ambalo amebainisha kuwa limeanzishwa kwa malekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kuona kuwa uwezeshaji wa wafanyabiashara una manufaa makubwa katika kukuza uchumi wa nchi hivyo dawati hilo limeanzishwwa kukabiliana na changamoto zinazojitokeza.
Nchota amesema kuwa dawati hilo litawaleta pamoja wafanyabishara katika suala la ukusanyaji kodi lakini pia kuhakikisha wanawasaidia kuwawekea mazingira mazuri ikiwemo kukutana na taasisi nyingine ili shughuli za biashara zisikwame kulingana na changamoto zinazojitokeza na wafanyabiashara wadogo waweze kukua.

Baadhi ya wafanyabiashara wa Mkoa Kigoma akiwemo Mwenyekiti wa Jumuia ya wafanyabiashara Mkoa Kigoma, Raymond Ndabiyegetse wametoa wito kwa mamlaka ya mapato (TRA) Mkoani humo kulitumia vizuri dawati la uwezeshaji la mamlaka hiyo kutimiza malengo yake kwa kuzifanyia kazi changamoto zinazowasilishwa ili kuongeza morali kwa wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Wafanyabishara, wenye viwanda na kilimo (TCCIA) Mkoa Kigoma, Prosper Guga amesema kuwa kumekuwa na changamoto kubwa kwa wafanyabiashara wanaovuka mpaka na wamefanya kazi kubwa kukabiliana na changamoto hiyo, hivyo wanaamini dawati hilo litawaleta pamoja katika kuzishughulikia changamoto za wafanyabiashara zinazojitokeza na kuzipatia ufumbuzi wa haraka ili kuwezesha biashara kukua na kukuza uchumi wa nchii.
Akizindua dawati hilo, Mkuu wa Mkoa Kigoma, Balozi Simon Sirro ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya Kigoma, Dk. Rashid Chuachua amesema kuwa dawati hilo ni maelekezo ya Raisi Samia hivyo wao kama wasaidizi wa Rais watasimamia kwa karibu kuona dawati hilo linatekeleza majukumu yake kikamilifu bila urasimu na kuchukua hatua kwa watendaji ambao wataenda tofauti na malengo ya dawati.