Joy FM

RC Sirro: Mipaka ya vijiji na kitalu cha uwindaji iwekwe alama

11 September 2025, 15:53

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro akizungumza na wananchi wa Kurugongo, Picha na Ofisi ya Mawasiliano Mkoa wa Kigoma

Wananchi wa vijiji vinavyopakana na enep la hifadhi ya Kitalu cha Uwindaji cha Makere – Uvinza wametakiwa kuheshimu mipaka iliyowekwa

Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro ameutaka uongozi wa Halmashauri ya Wiilaya ya Kasulu kutambulisha Mipaka ya vijiji vitano vinavyopakana na eneo la Hifadhi ya Kitalu cha Uwindaji cha Makere(FR)-Uvinza Open Area ndani ya wiki moja kuanzia Septemba 10, 2025. 

Maelekezo hayo yamekuja kufuatia uwepo wa mgogoro wa muda mrefu wa mipaka baina ya mwekezaji wa kitalu hicho chenye ukubwa wa Km.  za Mraba 2565 na wakazi wa vijiji vya Kagerankanda, Chekenya, Asante Nyerere, Mvinza na Kabulanzwili vinavyopakana na kitalu hicho. 

Akizungumza kupitia mkutano wa hadhara  na wakazi wa Kijiji cha Kurugongo kilichopo wilayani humo, Balozi Sirro ameutaka uongozi wa halmashauri kupitia Idara ya Ardhi kuhakikisha unabainisha na kuweka alama za wazi kwa kutumia ramani  rasmi iliyotumika kuanzisha vijiji hivyo na kitalu kwa kushirikiana na  uongozi wa vijiji hivyo. 

Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro
Wananchi wa Kijiji cha Kurugongo wakiwa katika mkutano wa Mkuu wa Mkoa Kigoma Balozi Simon Sirro, Picha Ofisi ya mawasiliano Mkoa

Sirro amesisitiza kuwa utekelezaji wa zoezi hilo unatakiwa kufanyika kwa muda uliopangwa ili kuruhusu wakazi wa vijiji hivyo kuendelea na shughuli za Kilimo sambamba na kuepusha usumbufu kwa mwekezaji katika kitalu. 

Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro

Abraham Rashid Mkazi wa kijiji cha Chekenya amesema changamoto inayowakabili ni uwepo wa baadhi ya wakazi katika maeneo hayo kushindwa kuitambua mipaka halisi na kujikuta wakivamia eneo tengefu la kitalu. 

Aidha Paschal Benga mkazi wa  kijiji cha kurugongo amepongeza hatua ya mkuu wa mkoa kuwafikia na kusikiliza changamoto zao huku akisistiza kuwa taratibu hizo za kisheria zitatatua changamoto hiyo.

Wananchi wa Kijiji cha Kurugongo wakiwa katika mkutano wa Mkuu wa Mkoa Kigoma Balozi Simon Sirro, Picha Ofisi ya mawasiliano Mkoa