Joy FM
Joy FM
2 September 2025, 11:09

Halmashauri ya Mji wa Kasulu Mkoani Kigoma imewataka wananchi kuzingatia usafi wa mazingira ili kuepuka mlipuko wa magonjwa
Na Hagai Ruyaila
Wananchi wa Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma wametakiwa kuongeza juhudi katika utunzaji wa mazingira kwa kuacha kutupa taka ovyo ili kuhakikisha wanaishi katika mazingira safi, salama na yenye afya bora.
Wito huo umetolewa na Afisa afya mazingira Halmashauri ya Mji Kasulu, Bw. Jovinus Mitoga kwaniaba ya mkuu wa kitengo cha usafi na udhibiti taka ambapo amesema ni muhimu kila mwananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za usafi wa mazingira katika maeneo yao, kwa kuzingatia utengaji wa taka ngumu na laini, pamoja na kushiriki katika kampeni za usafi zinazoratibiwa kila mwisho wa mwezi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Sido Bw. Jumanne Mustafa, amesema ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki katika shughuli za usafi, lakini bado kuna changamoto ya baadhi ya wananchi kuwa na uelewa mdogo kuhusu madhara ya uchafuzi wa mazingira.

Nao baadhi ya Wakazi wa Halmashauri ya Mji Kasulu wameeleza maoni yao kuhusu umuhimu wa usafi wa mazingira ambapo wamesema kuwa utunzaji wa mazingira ni jukumu la kila mmoja pia ni muhimu serikali ikaweka sheria kali kwa wanaokiuka.
Kwa ujumla, utunzaji wa mazingira katika Halmashauri ya Mji Kasulu unaonekana kuwa suala linalopaswa kupewa kipaumbele na jamii nzima, kwa kuwa mazingira bora ni msingi wa afya, uchumi na maendeleo ya jamii kwa ujumla.
