Joy FM
Joy FM
1 September 2025, 15:27

Serikali imesema itaendelea kuwasaidia wavuvi na wachakataji wa mazao ya uvuvi na kuwapatia masoko.
Na Kadislaus Ezekie
Wananchi mkoani Kigoma ambao wamejikita katika ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba kwa kufuga samaki aina ya sato wa Ziwa Tanganyika pamoja na wachakataji wa mazao hayo, wameiomba serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuwatafutia masoko makubwa ya ndani na nje ya nchi, baada ya kuongeza uzalishaji wa samaki hao.
Mradi wa ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba, umekuwa na tija kwa wafugaji ikiwa ni matokeo chanya baada ya serikali kuwawezesha vizimba hivyo kwa mkopo nafuu matokeo makubwa yakionekana kwa kuzalisha mazao mengi.
Wateja walionao ni wa ndani, soko ambalo halikidhi wingi wa mazao wanayopata kutoka katika vizimba wakati wa uvunaji wakiwa tayari wamevuna awamu ya kwanza.
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ikiwa katika ziara ya kukagua miradi ya serikali katika sekta hiyo, inaahidi kutafuta soko la uhakika sambamba na wawekezaji kuombwa kuja kuwekeza katika mradi huu.