Joy FM
Joy FM
28 August 2025, 10:51

Serikali imetoa wito kwa mabenki kubuni mipango mbalimbali ya utoaji wa elimu kwa umma na kuelekeza nguvu zaidi katika kukuza uelewa juu ya masuala ya kifedha pamoja na umuhimu wa kutumia huduma za benki.
Na Emmanuel Matinde – Kigoma
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango, amesema serikali inatambua mchango mkubwa wa Benki ya CRDB katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo nchini ikiwemo mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa SGR.
Dkt. Mpango amesema hayo leo Jumatano Agosti 27, 2025 wilayani Buhigwe wakati wa uzinduzi wa tawi la benki ya CRDB.
Amesema uzinduzi wa tawi hilo la benki ya CRDB ni hatua muhimu kwa wananchi wa Wilaya ya Buhigwe kukua kiuchumi, akieleza kwa muda mrefu walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za kibenki.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango, ameitaka benki ya CRDB kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wilayani Buhigwe ili waweze kunufaika na uwepo wa benki hiyo ikiwa na pamoja na fursa za mkopo zitakazowasaidia kuendeleza shughuli zao za kibiashara.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela, amesema benki hiyo inajivunia ushirikiano na serikali ambao unaiwezesha kuimarisha huduma zake katika maeneo mbali mbali nchini na kusogeza huduma za kifedha karibu na wananchi.