Joy FM
Joy FM
27 August 2025, 13:56

Idadi ya watoto wa kike wanaosoma masomo ya sayansi imeendelea kuongezeka na hiii ni kutokana na jitihadi mbalimbali za Serikali na wadau wengine katika kuwahamasisha kupenda masomo ya sayansi
Na Hagai Ruyagila
Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma imefanikiwa kutumia wataalamu wa elimu kwa kushirikiana na jamii katika kuongeza hamasa kwa watoto wa kike kusoma masomo ya sayansi.
Hayo yameelezwa na Afisa Elimu ya watu wazima sekondari halmashauri ya Mji Kasulu Gaspar Kulikiza wakati akiwasilisha taarifa ya idara ya elimu kwa wadau wa elimu mkoa wa Kigoma kikao kilichofanyika mjini Kasulu.
Amesema wataalamu wa elimu wamekuwa wakifanya mikutano ya hamasa shuleni na kwenye jamii, wakitoa elimu juu ya umuhimu wa wasichana kujihusisha na masomo ya sayansi.

Aidha Kulikiza amesema jamii imehusishwa kikamilifu kupitia vikao vya wazazi na walezi, vikundi vya wanawake, pamoja na viongozi wa mitaa ili kuondoa dhana potofu na mila zinazoweza kuwakatisha tamaa watoto wa kike kufuatilia masomo hayo.
Amesema juhudi hizi zimeanza kuzaa matunda, ambapo baadhi ya shule zimeonyesha ongezeko la idadi ya wanafunzi wa kike wanaochagua masomo ya sayansi, pamoja na kuongeza ufaulu katika masomo hayo.
Kwa upande wake, Afisa elimu ya watu wazima mkoni Kigoma Fausta Akaro ambaye pia ni mratibu wa miradi ya UNICEF inayoshughurika na watoto walioko nje ya mfumo rasmi amesema lengo kubwa la serikali ni kuhakikisha watoto wote wanapata elimu ili kufikia ndoto zao.