Joy FM

Maafisa elimu watakiwa kusimamia elimu ya MEMKWA

25 August 2025, 13:00

Baadhi ya maafisa elimu kutoka halmashauri za Mkoa wa Kigoma, Picha na Hagai Ruyagila

Serikali Mkoani Kigoma imesema itaendelea kuhamasisha wananchi kuhakikisha wanaweka mazingira wezeshi kwa ajili watoto hasa wa kike ili waweze kupata elimu.

Na Hagai Ruyagila

Maafisa elimu na Waalimu kutoka halmashauri mbalimbali za mkoa wa Kigoma wametakiwa kuhakikisha wanazingatia na kutumia kwa vitendo mafunzo na semina wanazopatiwa ili kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuwaandikisha watoto walio nje ya mfumo rasmi wa elimu (MEMKWA), hususan watoto wa kike, kwa lengo la kuwarejesha shuleni na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika masomo ya sayansi.

Wito huo umetolewa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Deogratius Sangu, wakati akifunga kikao cha tathmini ya utekelezaji wa miradi ya elimu mkoani humo kilicho husisha maafisa elimu kutoka halmashauri zote za mkoa wa Kigoma kikilenga kuimarisha juhudi za kuongeza ushiriki wa wanafunzi wa kike katika elimu, hasa katika masomo ya Sayansi

Sangu amesema mpango wa MEMKWA ni nyenzo muhimu ya kutoa fursa ya pili kwa watoto waliokatishwa masomo au ambao hawakuwahi kuandikishwa kabisa, hivyo ni lazima utekelezwe kwa ufanisi na kwa ushirikiano wa karibu baina ya wadau wote wa elimu.

Sauti ya Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Deogratius Sangu
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Deogratius Sangu, Picha na Hagai Ruyagila

Kwa upande wake, Afisa elimu ya watu wazima mkoa wa Kigoma Fausta Akaro ambaye pia ni mratibu wa miradi ya UNICEF inayoshughurika na watoto walioko nje ya mfumo rasmi amebainisha lengo la kikao hicho ni kuangalia namna ya uendeshaji wa madarasa ya MEMKWA katika halmashauri hizo na kuhakikisha watoto walioacha shule wanarudi shule.

Sauti ya Afisa elimu ya watu wazima mkoa wa Kigoma Fausta Akaro

Mwenyekiti wa maafisa elimu mkoa wa Kigoma Lawi Kajanja amesema wameendelea kuhamasisha zaidi kuhakikisha mtoto wakike anasoma pasipo kumuacha mtoto wakiume na wanaendelea kuboresha miundombinu ya sekta ya elimu.

Sauti ya Mwenyekiti wa maafisa elimu mkoa wa Kigoma Lawi Kajanja

Baadhi ya Maafisa elimu wamesema tathmini hiyo itakwenda kuongeza chachu katika sekta ya elimu mkoani Kigoma.

Sauti ya baadhi ya Maafisa elimu