Joy FM
Joy FM
19 August 2025, 16:53

Ujenzi wa chuo kikuu cha afya na Sayansi shirikishi MUHAS kampasi ya Kigoma unatajwa kuongeza tafiti na matibabu kwa kwa wananchi wa mkoa wa Kigoma na maeneo mengine.
Na Mwandishi wetu
Serikali ya Mkoa wa Kigoma imesema kukamilila kwa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Kampasi ya Kigoma kunatarajiwa kuongeza chachu katika kufanyika kwa tafiti za kiafya na matibabu ili kukabiliana na magonjwa kutokana na mkoa kupakana na nchi jirani ambapo mara kadhaa zimetolewa taarifa za uwepo maradhi ya mlipuko.
Akizungumza mara baada kukagua mradi wa Ujenzi wa Chuo hicho, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Kanali Michael Ngayalina amesema chuo hicho kitakapokamilika kitaondoa adha kwa wakazi kufuata matibabu ya kibingwa nje ya Mkoa na kuongeza kasi ya udhibiti na matibabu ya maradhi mbalimbali.
Amesema sambamba na utoaji wa huduma za kiafya, chuo kitachangia kuimarisha Uchumi wa wakazi hivyo Serikali ya Mkoa itaendelea kutoa ushirikiano na Taasisi hiyo ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati.

Upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo hicho Appolinary Kamuhabwa amesema ujenzi wa Chuo hicho unaotekelezwa chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Uchumi (HEET) umefikia Asilimia 19 huku ukitarajiwa kukamilika ifikapo Juni 2026.
Amesema matarajio ni kwamba Kampasi hiyo itakapokamilika itaweza kuchukua wanafunzi 6000 ambapo kwa kuanza itapokea wanafunzi 300 huku bweni linalojengwa katika hatua ya awali likiwa na uwezo wa kupokea wanafunzi 111.
Aidha amezitaja baadhi ya faida ya uwepo wa chuo hicho mkoani Kigoma kuwa ni kuongezeka kwa utalii tiba nchini sambamba na ongezeko la wawekezaji na wafanyabiashara wa huduma kutoka maeneo ya ndani na nje ya mkoa pamoja na nje ya nchi.
