Joy FM
Joy FM
28 July 2025, 17:15

Waziri wa Mendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Doroth Gwajima amezindua kampeni ya kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto na kuwataka viongozi wa mikoa nchini kuwachukulia hatua za kisheria wagaga wa jadi ambao wamekuwa wakipiga ramli zinazochochea vitendo hivyo.
Na Josephine Kiravu
Imeelezwa kuwa takribani watoto 47 katika Manispaa ya Kigoma Ujiji wamefanyiwa ukatili wa kingono katika kipindi cha miezi 3 huku mikakati kadhaa ikiendelea kuwekwa ili kutokomeza vitendo hivyo.
Hayo yameelezwa na Waziri Maendeleo ya jamii, Jinsia na makundi maalum Doroth Gwajima wakati wa uzinduzi wa kampeni ya badilika tokomeza ukatili inayotekelezwa na Shirika la Enabel kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania yenye lengo la kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana Mkoani Kigoma.

Hata hivyo amewataka viongozi kuweka mikakati ya kukabiliana na vitendo vya ukatili ili kuwanusuru watoto ambao wamekuwa wakibakwa na kulawitiwa.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Wilaya ya Kigoma Mganwa Nzota ameeleza mikakati ya kukabiliana na vitendo hivyo huku akiwataka viongozi hasa wa ngazi za chini kushirikiana na wananchi kufichua wanaotekeleza vitendo vya ukatili.
Awali akieleza kuhusu madhumuni ya mradi huo, Mkurugenzi mkaazi Enabel Koen Goekint amesema kampeni hiyo inatarajia kuwafikia wanamabadiliko 150,000 kwa mkoa wa Kigoma ifikapo 2027 ambao watakuwa tayari kubadili fikra mitazamo na mienendo yao juu ya vitendo vya ukatili.
Na hapa baadhi ya wazazi wanaeleza nini kifanyike huku suala la uchumi likitajwa kuchangia vitendo hivyo kuongezeka.
Kampeni ya Badilika tokomeza ukatili inatekelezwa katika halmashauri tano za mkoa wa Kigoma ambazo mradi wa wezesha binti unaendelea kutekelezwa.
