Joy FM

Tusiwafiche watoto wenye ulemavu-DC Kasulu

28 July 2025, 09:55

Baadhi ya watoto wenye ulemavu pamoja na wazazi wao katika kongamano la elimu, Picha na Hagai Ruyagila

Wazazi na walezi wenye watoto wenye ulemavu wameshauriwa kutowafisha watoto wenye mahitaji maalumu kwa kufanya hivyo ni kuwanyima haki zao msingi.

Na Hagai Ruyagila

Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu, ametoa wito kwa wazazi na walezi wilayani humo kutowaficha watoto wao wenye mahitaji maalumu, bali wawapeleka shule ili wapate elimu itakayowawezesha kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa.

Kanali Mwakisu ametoa kauli hiyo wakati akihutubia Kongamano la Kielimu kwa Wanafunzi Wenye Mahitaji Maalumu pamoja na wazazi wao lililofanyika mjini Kasulu.

Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu, Picha na Hagai Ruyagila

Amesisitiza kuwa elimu ni haki ya msingi kwa kila mtoto, wakiwemo watoto wenye ulemavu, na kwamba serikali ipo tayari kutoa huduma zote muhimu kuhakikisha watoto hao wanapata elimu stahiki.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu

Mratibu wa Kongamano hilo ambaye pia ni mwalimu wa Shule ya Msingi Kisuma Mwalimu Yusufu Ibrahimu akisoma risala kwa mgeni rasmi ameeleza malengo ya kongamano hilo na kubainisha baadhi ya mafanikio yaliyopatikana hadi sasa pamoja na changamoto zinazowakabili watoto wenye mahitaji maalumu katika mchakato wa kupata elimu.

Sauti ya mwalimu wa Shule ya Msingi Kisuma Mwalimu Yusufu Ibrahim

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wenye Ulemavu wa Viungo (CHAWATA) Wilaya ya Kasulu, Bi. Eva Gwisangura, ameiomba serikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kuwatambua na kuwawezesha watu wenye mahitaji maalumu ili wapate haki zao kama wengine.

Sauti ya Mwenyekiti wa Chama cha Wenye Ulemavu wa Viungo Wilaya ya Kasulu

Naye mwakilishi wa wazazi wa watoto wenye mahitaji maalumu, Bi. Elizabeth Kamenya, ameishukuru serikali kwa juhudi zake na kuomba iendelee kuwapatia fursa mbalimbali zitakazosaidia kuinua hali za familia zao na kuwasaidia watoto hao kutimiza ndoto zao.

Sauti ya mwakilishi wa wazazi wa watoto wenye mahitaji maalumu,
Mwenyekiti wa Chama cha Wenye Ulemavu wa Viungo (CHAWATA) Wilaya ya Kasulu, Bi. Eva Gwisangura, Picha na Hagai Ruyagila

Kongamano hili linaendelea kuwa jukwaa muhimu la kuelimisha, kuhamasisha, na kuchochea mabadiliko chanya katika kuhakikisha usawa na ujumuishaji wa watoto wenye mahitaji maalumu katika sekta ya elimu.

Kongamano hilo limebeba kaulimbiu isemayo: “Unyanyasaji dhidi ya watu wenye ulemavu sasa basi, tupewe haki kama wengine.”