Joy FM
Joy FM
18 July 2025, 13:11

Kilimo cha zao la mchikichi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma kimeanza kuleta mafanikio kiuchumi kwa wakulima kufuatia usambazaji wa mbegu bora aina ya Tenera.
Na Emmanuel Kamangu
Wananchi wilayani Kasulu mkoa wa Kigoma wametakiwa kuchangamkia fursa ya kilimo cha zao la chikichi kwa tumia mbegu bora aina ya tenera, mbegu zinazotajwa kuwa na tija na stahimilivu kwa magonjwa.
Wito huo umetolewa na Kaimu Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Halamashauri ya Wilaya ya Kasulu Bw. Masumbuko Kelemwa wakati akizungumza na waandishi wa habari kufuatia ziara ambayo imefanyika katika Kijiji cha Kiungwe, Kata ya Kitanga kuona maendeleo ya mashamba ya chikichi ambayo yanalimwa na wananchi kwa mbegu wanazopewa na halmashauri hiyo ikiwa ni mkakati wa serikali wa kuhakikisha zao hilo linawakwamua kiuchumi.
Aidha Bw. Kelemwa amewataka wananchi wilayani Kasulu kuondokana na kilimo cha mazoea badala yake wajikite kulima kilimo chenye tija kwa maendeleo zaidi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kiungwe Bw. Enock Mugama akiongea kwa niaba ya wananchi amesema kutokana na upatikanaji wa mbegu bora pamoja na mafunzo ya kilimo wanayoendelea kupewa imekuwa chachu ya wakulima wengi kuwa na matumaini ya kujikita katika zao la mchikichi.
Hatua hii imechochea mageuzi makubwa kutoka kilimo cha mazoea kwenda kilimo cha kibiashara jambo linalotarajiwa kuongeza tija, kipato na ustawi wa wananchi wa wilaya hiyo.
