Joy FM

Watu 10 wahukumiwa maisha jela kwa mauaji

11 July 2025, 09:02

Mahakama Mjini Bujumbura ikiwa inasikiliza kesi ya watuhumiwa waliohusika katika mauwaji ya watu sita, Picha na Bukuru Daniel

Imani za kishirikina zasababisha watuhumiwa kufungwa kifungo cha maisha jela.

Na Bukuru Daniel

Mahakama kuu ya Bujumbura imewahukumu watu kumi kifungo cha maisha jela kwa kuhusika katika mauaji ya kutisha ya wakaazi sita katika kijiji cha Gasarara wilaya ya Nyabiraba, Mkoa wa Bujumbura. Mauaji hayo yaliyotokea wiki iliyopita yanadaiwa kusababishwa na tuhuma za uchawi.

Ghasia hizo zilizuka wiki iliyopita baada ya mfanyakazi wa kanisa katoliki na paroko mmoja katika kijiji hicho kuugua katika mazingira ya kutatanisha. 

Waathiriwa walipigwa, kupigwa mawe, na wengine kuchomwa moto ambapo watu sita wanaume wanne, mwanamke mmoja na msichana mdogo walikufa papo hapo.

Polisi walitumwa katika eneo hilo na kufanikiwa kuwaondoa manusura watatu, ingawa wawili kati yao walifariki baadaye kutokana na majeraha. Mauaji hayo yalizua ghadhabu na kulaaniwa haraka na mamlaka za kitaifa na makundi ya kutetea haki za binadamu.

Watu kumi na sita walikamatwa kufuatia uchunguzi aliofanyika ambapo mahakama ilitoa hukumu ya kifungo cha maisha jela kwa wanaume kumi waliopatikana na hatia ya kupanga na kutekeleza mauaji hayo. 
Wengine wawili walihukumiwa kifungo cha miaka 20 kwa kuhusika katika mauaji ya dada wawili. Watu wengine wanne walihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kwa kushindwa kuingilia kati wakati wa shambulio hilo huku washukiwa waliosalia wakiachiliwa huru.