Joy FM

Ubalozi wa Tanzania nchini Burundi wazindua kampeni ya matibabu bure

10 July 2025, 13:09

Baadhi ya waandishi wa habari Nchini Burundi wakiwa katika Mkutano na Balozi wa Tanzania Nchini Burundi, Picha na Bukuru Daniel

Madaktari bingwa kutoka nchi Tanzania wanatarajia kuweka kambi ya matibabu katika maeneo mbalimbali nchini Burundi kwa lengo la kutoa matibabu kwa wananchi Burundi.

Na Bukuru Daniel

Ubalozi wa Tanzania nchini Burundi kwa kushirikiana na wizara ya afya na VVU/UKIMWI nchini Burundi pamoja na Hospitali ya Benjamin William Mkapa nchini Tanzania wameandaa kampeni kwa lengo la kutoa matibabu bora kwa Warundi wenye magonjwa mbalimbali.

Kwa mujibu wa Balozi wa Tanzania nchini Burundi Mhe.Gelasius Gaspar Byakanwa,  madaktari hao watatibu magonjwa mbalimbali yakiwemo ulemavu wa miguu unaotokana na ajali au magonjwa mengine, watafanya upasuaji wa mishipa ya ubongo na uti wa mgongo, magonjwa ya macho na moyo.

Sauti ya Balozi wa Tanzania nchini Burundi Mhe. Gelasius Gaspar Byakanwa
Balozi wa Tanzania nchini Burundi Mhe. Gelasius Gaspar Byakanwa, Picha na Bukuru Daniel

Mhe. Byakanwa amesema kuanzia tarehe 14 hadi 18 Januari 2025, madaktari hao watafanya kazi katika hospitali kuu ya Gitega. Kuanzia tarehe 21 hadi 25 Julai 2025, madaktari hao watafanyia kazi katika Hospitali ya Prince Rudoviko Rwagasore mjini Bujumbura.

Sauti ya Balozi wa Tanzania nchini Burundi Mhe. Gelasius Gaspar Byakanwa

Byakanwa pia alieleza kuwa zoezi hilo la matibabu ni sehemu ya uimarishaji wa mahusiano ya kusaidiana kati ya Burundi na Tanzania, pamoja na mipango ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ya kusogeza huduma bora za afya karibu na wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.