Joy FM
Joy FM
4 July 2025, 16:05

Kubadili taka kuwa fursa ni mchakato wa ubunifu unaohusisha matumizi ya maarifa, teknolojia na ujasiriamali ili kutumia taka kama rasilimali yenye thamani badala ya kuona taka kama uchafu.
Na Josephine Kiravu
Zaidi ya wafanyabiashara 250 na wadau mbalimbali wa mazingira na uchumi Mkoani Kigoma wamepatiwa mafunzo ya namna ya kubadili taka na kuwa fursa sambamba na kulinda maji ya Ziwa Tanganyika.
Wafanyabiashara hao pamoja na wadau mbalimbali wamekutana kwa lengo la kupata mafunzo ambayo yameandaliwa shirika la CRS kwa kushirikiana na CARITAS pamoja na TCCIA chini ya mradi wa The Voices.

Meneja mradi wa The Voices Robert Adrian amesema lengo la mafunzo hayo ni kubadili taka kuwa fursa pamoja na kutunza maji ya ziwa Tanganyika kwa kuzuia uchafuzi wa mazingira na kutumia vyema dampo la msimba kwenye ukusanyaji wa taka.
Kwa upande wake, Katibu wa Chemba ya biashara mkoani Kigoma (TCCIA) Prosper Guga amesema changamoto kubwa inayowakabili wajasiriamali ni elimu hivyo kupitia mafunzo hayo yatasaidia kuwafungua na kutumia taka kama fursa.
Nao baadhi ya wadau waliohudhuria katika mafunzo hayo akiwemo Genoviva Mtiti wamesema awali taka hizo ikiwemo chupa za maji zilionekana kama uchafu lakini kupitia elimu waliyoipata itasaidia kwa kiasi kikubwa wajasiriamali na wafanyabiashara kuchukulia kama fursa kwao.
Kwa mujibu wa meneja mradi wa The Voice tayari imetengwa ruzuku kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali na wafanyabisahara huku akizitaka pia taasis za fedha kufungua milango ya mikopo ili kuwawezesha kuendesha shughuli zao.