Joy FM

Walimu watakiwa kufanya tathmini ya mitihani

3 July 2025, 16:06

Maafisa elimu kata na walimu wakuu wa shule za msingi Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Picha na Emmanuel Kamangu

Ili kupandisha ufaulu kwa wanafunzi, Walimu na Maafisa elimu wameshauri kuffuatilia nakufanya tathimini kwa wanafunzi waliofanya vibaya mitihani yao.

Na Emmanuel Kamangu

Maafisa elimu kata na walimu wakuu wa shule za msingi Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu wametakiwa kufanya tathmini ya mtihani wa Moko ili kuwatambua wanafunzi waliopata alama za chini na kuweka mikakati ya kuwawezesha kuongeza ufaulu.

Akizungumza kwenye kikao cha tathmini ya elimu leo Julai 2, 2025, Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri hiyo, Elestina Chanafi, amesisitiza umuhimu wa kusaidia wanafunzi waliopata alama D na E kufikia C hadi A.

Sauti ya Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri hiyo, Elestina Chanafi

Aidha, amewataka walimu wakuu na maafisa elimu kuhakikisha matumizi sahihi ya mifumo ya serikali katika maeneo ya taaluma, utumishi, na fedha. Amesisitiza umuhimu wa kusimamia miradi inayoendeshwa mashuleni ili ikamilike kwa wakati na kuonyesha thamani halisi ya fedha zinazotumika.

Afisa Elimu Msingi halmashauri ya wilaya ya Kasulu Bi.Elestina Chanafi, Emmanuel Kamangu

Naye Afisa Uthibiti Ubora wa Shule, Leonsia Sugwejo, amesema tathmini kwa njia ya video imeonyesha mafanikio makubwa, ikiwemo kuibuka kwa Mwalimu Joseph Masika wa Shule ya Sekondari Kitanga kuwa miongoni mwa washindi wa juu kitaifa kwenye somo la Fizikia.

Afisa Ajira na Maendeleo ya Walimu (TSC) Wilaya ya Kasulu, Kazimoto Nkomoli, amewataka walimu kuzingatia matumizi sahihi ya mfumo wa E-Utendaji ili kuepuka madhara ya kutotambuliwa kiutumishi au kukosa fursa za maendeleo.

Sauti ya Afisa Uthibiti Ubora wa Shule, Leonsia Sugwejo

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Shule Bora Mkoa wa Kigoma, Celestine Bukango, amehimiza shule kuwa na dira ili kuhakikisha shughuli zote zinaendeshwa kwa mwelekeo thabiti unaoakisi malengo ya shule.

Sauti ya Mratibu wa Mradi wa Shule Bora Mkoa wa Kigoma, Celestine Bukango