Joy FM

Jamii yatakiwa kufanya usafi mara kwa mara Kasulu

30 June 2025, 14:37

Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Kasulu akishirikiana na watumishi wa halmashauri hiyo sambamba na baadhi ya Wananchi wakifanya usafi wa mazingira.

Jamii imeshauriwa kuzingatia suala la utunzaji wa mazingira ili kuhakikisha maeneo yao yanakuwa safi na kudhibiti magonjwa ya mlipuko.

Na Hagai Ruyagila

Halmashauri ya Mji wa Kasulu imezindua rasmi programu ya usafi wa mazingira kwa lengo la kuhamasisha jamii kuwa na utamaduni wa kufanya usafi wa mara kwa mara, ili kuepuka magonjwa ya mlipuko na kuufanya mji huo kuwa safi na wa kuvutia kama ilivyo kwa miji mingine nchini.

Akizindua programu hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Mwalimu Vumilia Simbeye, amesema lengo kuu ni kuhakikisha mji huo unaendelea kuwa safi na salama kwa afya ya wakazi wake.

Sauti ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Mwalimu Vumilia Simbeye

Aidha, Mwl. Simbeye amewaomba wananchi wote wa Halmashauri ya Mji Kasulu kushiriki kikamilifu katika shughuli za usafi zinazofanyika kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi, kwa kushirikiana na serikali katika kusafisha maeneo mbalimbali ya mji huo.

Sauti ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Mwalimu Vumilia Simbeye

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi waliojitokeza kushiriki katika zoezi hilo wameeleza kuwa wanaunga mkono juhudi za serikali na wako tayari kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo kila litakapoitishwa, wakisisitiza kuwa usafi ni jukumu la kila mwananchi.

Sauti ya baadhi ya wananchi

Zoezi hilo la usafi wa mazingira limeanza rasmi katika eneo la barabara kuu (Highway) na kuendelea hadi katika stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani, ikiwa ni ishara ya kuanza kwa utekelezaji wa programu hiyo muhimu.

Baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu wakifanya usafi wa mazingira mjini Kasulu