Joy FM
Joy FM
9 June 2025, 16:30

Jamii mkoani Kigoma imetakiwa kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili watu wenye ualbino huku wakitakiwa pia kuondokana na imani potofu za kishirikina kuhusu watu hao.
Na Josephine Kiravu
June 13 ya kila mwaka dunia huadhimisha siku ya kimataifa ya uelewa wa watu wenye ulemavu wa ngozi ambapo dhamira kuu ni kutambua umuhimu wa kulinda haki za watu wenye ualibino kwa wakati huu ambapo baadhi yao wamekuwa wakiuwawa kwa imani za kishirikina.
Kwa mwaka huu maadhimisho hayo Kitaifa yanatarajia kufanyika mkoani Kigoma ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa waziri mkuu Kassim Majaliwa.
Akizungumza na wanahabari, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Jenerali mstaafu wa jeshi la zimamoto na uokoaji Thobias Andengenye amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye maadhimisho hayo ili kupata uelewa na elimu kuhusu watu wenye ualibino.
Ameongeza kuwa Mkoa utaendelea kuwathamini na kuwalinda watu wenye ualibino kwa kuhakikisha wanapata haki zao za msingi ikiwemo elimu.
Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha watu wenye ualubino Tanzania Godson Mollel licha ya kuishukuru Serikali kwa kuwathamini lakini ameiomba jamii kuwa mstari wa mbele kuwalinda na kuachana na imani potofu zinazopelekea wenzao kuuwawa.
Kilele cha maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya uelewa kuhusu ualibino itakuwa June 13 mwaka huu ikiwa na kauli mbiu isemayo kushiriki katika uchaguzi ni haki, kuchaguana, kuchaguliwa na kulinda haki za watu wenye ualibino.