

19 February 2025, 09:51
Kaimu Mkuu wa Wilaya Kasulu ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya Buhigwe Kanali Michael Ngayalina amesema watumishi wa umma hawana budi kuzingatia weledi na taaluma yao katika kuwatumikia wananchi.
Na Hagai Ruyagila
Watumishi wa Umma katika halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma wametakiwa kufanya kazi kwa uweledi ili kutimiza malengo ya serikali ya awamu ya sita kwa kutoa huduma bora kwa jamii.
Wito huo umetolewa na Kaimu Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanal Michael Ngayalina wakati akizungumza na watumishi wa umma, kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Kasulu na madiwani wa halmashauri ya Mji Kasulu katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.
Kanal Ngayalina amesema watumishi wa umma wajibu wao ni kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa jamii ili wananchi waweze kuiamini serikali yao inayowaongoza pasipo changamoto yoyote.
Kwa upande wake katibu wa chama cha demokrasia na Maendeleo CHADEMA wilaya ya Kasulu Emmanuel Simon amesema ni vyema Mkuu wa wilaya ya Kasulu aendelee kufuatilia na endapo atabaini changamoto kwa mtumishi wa umma katika halmashauri hiyo aweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Nao baadhi ya watumishi wa umma kutoka halmashauri ya hiyo akiwemo Mganga mkuu wa halmashauri ya Mji Kasulu Dkt Peter Janga na Afisa Ardhi wa halmashauri ya Mji Kasulu Pesha Jackson wamesema wamepokea maagizo hayo ili kufanikisha shughuli za serikali zinafanikiwa kwa kutoa huduma bora kwa jamii.