Kasulu mji yakabidhi milioni 34 kwa vikundi vitano
24 January 2025, 12:48
Utoaji wa mikopo kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu inatajwa kuwa mkombozi kwa wanufaika wa mikopo hiyo kiuchumi.
Na Hagai Ruyagila
Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma imekabidhi hundi ya mkopo wa zaidi ya shilingi milioni 34 kwa vikundi 5 kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa utoaji mikopo hiyo kwa awamu ya kwanza ambayo imeanza kutolewa mwezi januari mosi hadi januari 30 Mwenyekiti wa halmashauri ya Mji Kasulu Bw Noel Hanura amewataka wanufaika wa mikopo hiyo kuzitumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa kwa ajili ya kuleta maendeleo ya familia zao.
Hanura amesema endapo wanafaika hao wa mikopo ya asilimia 10 watarejesha mikopo hiyo kwa wakati uliokusudiwa wataendeleo kunufaika zaidi na mikopo hiyo inayotokana na mapato ya ndani ya halmashauri ili kuwasidia kuinuka kiuchumi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Kasulu Mwl, Vumilia Simbeye amesema mikopo hiyo inayotokana na papato ya ndani ya halmashauri itawasaidia kutimiza malengo yao waliyojiwekea na kuinua uchumi wa jamii katika kufanya shughuli za maendeleo.
Afisa maendeleo halmashauri ya Mji Kasulu Bw Godfrey Jeremia amesema tayari halmashauri imetenga zaidi ya shilingi milioni 300 ya mkopo kuhakikisha vikundi vilivyokidhi vigezo vinapatiwa mikopo katika awamu ya pili.
Nao baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo wameishukuru serikali na kueleza namna itakavyowasaidia kuendesha maisha yao.