Wavuvi watakiwa kutumia zana zilizoainishwa kwa ajili ya uvuvi
21 January 2025, 16:07
Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika ziwa Tanganyika wametakiwa kutumia zana za uvuvi zilizoruhusiwa na kuainishwa wakati wa kuvua ili kulinda mazalia ya samaki.
Na Josephine Kiravu – Kigoma
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Dkt. Ashatu Kijaji amezindua kiwanda cha kuchakata Samaki na dagaa cha Lifa company Limited pamoja na kutembelea vizimba vya kufugia samaki eneo la Katabe Beach na kuwataka wananchi kutumia zana zilizoainishwa kwa ajili ya uvuvi ili kuendelea kulinda mazao yatokanayo na ziwa Tanganyika kwa manufaa ya kizazi kijacho.
Awali akitoa Taarifa ya kuhusu Maendeleo ya Sekta ya Uvuvi mkoani Kigoma, Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa amesema soko la mazao ya Samaki kwa mkoa wa Kigoma limeendelea kukua na kuleta tija kwa wafanyabiashara wa bidhaa hiyo.
Kwa upande wake, mkuu wa wilaya ya Kigoma Dr Rashid Chuachua kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Kigoma amesema kwa kushirikiana na wataalam wa uvuvi, mkoa unaendelea kuhamasisha wananchi kujikita katika uvuvi wa kutumia vizimba ili kuongeza uzalishaji wa samaki pamoja na kulinda Mazingira katika Ziwa Tanganyika na kulifanya kuwa endelevu.
Naye Mkurugenzi wa kiwanda cha Lifa products company Limited amesema changamoto zinazowakabili kwa sasa ni upatikanaji hafifu wa mazao ambapo ameiomba Wizara ya Uvuvi kuona haja ya kuwekeza kwenye uwekezaji wa vizimba Kwa ajili ya ufugaji wa mazao ya samaki.
Waziri wa mifugo na Uvuvi Dr Ashatu Kijaji amesema uwekezaji unaondelea nchini wa ujenzi wa viwanda Kwa ajili ya uchakataji wa mazao utasaidia kutoa ajira Kwa vijana, akina mama na wavuvi na kwamba kwa kiwanda ambacho kimezinduliwa leo kwa mwaka uchakataji wake unatarajiwa kuwa tani 432.