Askofu Mkuu anglikana ataka wananchi kushiriki uchaguzi mkuu
20 January 2025, 17:05
Wakati Taifa likielekea kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani viongozi wa dini wameendelea kuhamasisha wananchi kushiriki katika uchaguzi huo ambao ndio utatoa mwelekeo wa miaka mitano ijayo.
Na Hagai Ruyagila
Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Fabian Maimbo mndolwa amewataka wananchi Mkoani Kigoma kushiriki katika uchaguzi Mkuu Mwaka huu kwa kudumisha amani na kuwachagua Viongozi wenye uwezo wa kuleta maendeleo.
Askofu Mndolwa amesema hayo wakati akiongoza ibada ya takatifu ya kutabaruku kanisa kuu la Mt. Andrea Anglikana Kasulu mjini.
Amesema kuelekea katika uchaguzi mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais Wananchi wanatakiwa kuwachagua viongozi wenye hofu ya Mungu ambao watakuwa na uwezo wa kuleta maendeleo katika maeneo yao na kulinda amani ya Nchi.
Aidha Askofu mndolwa ameipongeza serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya barabarani katika maeneo mbalimbali nchi na kwamba wataendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Akimuwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Philipo Mpango, katika hotuba yake Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanali Isaac Mwakisu amewaomba viongozi wa dini nchini kuliombea taifa ili Mchakato wa uchaguzi mkuu mwezi oktoba mwaka huu ufanyike kwa amani.
Kwa upande wake askofu wa kanisa la anglikana dayosisi ya western Tanganyika Mhashamu Emmanuel Bwatta amemshukuru Mungu, waumini na wadau wa maendeleo kwa namna walivyosaidia kufanikisha ukarabati mkubwa wa kanisa kuu la Mtakatifu Andrea.
Mpaka sasa ukarabati wa kanisa la Mt. Andrea umegharia kiasi cha tsh milioni 325 licha ya kutokukamilika kwa asilimia mia moja hivyo ili kukamilika kwa asilimia mia moja zinatakiwa tsh milioni 125.