DC Kigoma aagiza watuhumiwa wa ubakaji kukamatwa
16 January 2025, 11:03
Vitendo vya ubakaji vimeendelea kutokea licha ya elimu kutolewa na baadhi ya watuhumiwa wakichukuliwa hatua.
Na Josephine Kiravu
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dr Mohamed Rashid Chuachua amemuagiza mkuu wa polisi wilaya ya Kigoma kuwakamata na kuhakikisha wanapelekwa mahakamani watuhumiwa wa ubakaji akiwemo mtuhumiwa ambaye amembaka mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya sekondari Rusimbi na kumsababishia ujauzito hali ambayo imemfanya kukatisha ndoto zake za masomo.
Baba wa mwanafunzi ambaye mpaka sasa ndoto zake zimezimika baada ya kupata ujauzito akiwa kidato cha tatu anaeleza kuwa hakutarajiakama mwanae atafanyiwa ukatili huo.
Mzazi huyu ambaye anaonekana kuumizwa na kitendo alichofanyiwa mwanae na kijana ambaye amemtaja ni dereva pikipiki anasimulia namna alivyogundua mwanae ni mjamzito na hatua ambazo hadi sasa amezichukua.
Tukio hilo limewaibua baadhi ya wadau akiwemo Kiongozi wa chama na NLD ambae amelitaka jeshi la polisi kuwakamata na kuwapatia adhabu watuhumiwa wa vitendo vya ukatili.
Awali akifungua kikao cha kamati ya ushauri ya maendeleo wilaya ya Kigoma mkuu wa wilaya ya kigoma Mh Dr Rashid Chuachua aliwataka wajumbe wa kikao hicho kuona haja ya kujadili namna gani bora ya kutokomeza vitendo vya ukatili.
Akihitimisha kikao hicho mkuu wa wilaya licha ya kumtaka mkuu wa polisi wilaya ya Kigoma kuwakamata watuhumiwa waliofanya ukatili na ambao kesi zao hazijapelekwa mahakamani na kuwataka akina baba kuwa mstari wa mbele kusimamia maadili kwa watoto.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na shirika la kuhudumia watoto duniani UNICEF karibu watoto milioni 400 wanakabiliwa na ukatili wa kimwili na kisaikolojia majumbani na kati yao asilimia 60 wapo chini ya miaka 5.