Viongozi serikali za mitaa watakiwa kutatua changamoto za wananchi
7 January 2025, 12:41
Viongozi wa Serikali za mitaa katika Halmashauri ya mji wa Kasulu Mkoani Kigoma wametakiwa kusimamia na kutatua changamoto za wananchi katika maeneo yao.
Na Hagai Ruyagila – Kasulu
Wenyeviti wa serikali za mitaa wa halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma wametakiwa kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali katika mitaa yao ili kutatua changamoto za wananchi kwa wakati.
Akifungua semina ya siku 2 ya mafunzo ya uongozi kwa wenyeviti wa mitaa 108, Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Kasulu Mwl, Vumilia Simbeye amewataka wenyeviti wa mitaa katika halmashauri hiyo kushirikiana na watendaji wa mitaa na kata kufuatilia miradi inayotekelezwa katika maeneo yao.
Mwl, Simbeye amesema serikali inatenge fedha kwa ajili ya kuleta maendeleo kwa wananchi na kwamba ni jukumu la kila kiongozi kwa nafasi yake kuhakikisha anasimamia ili miradi hiyo iweze kukamilika kwa wakati.
Kaimu kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU wilaya ya Kasulu Alpha Eliatosha amesema mwenyekiti wa serikali ya mtaa anatakiwa kujiepusha na vitendo vya rushwa pamoja na kutambua mipaka ya majukumu yake na kuacha tabia ya kusuruhisha migogoro ya ardhi kwa kuwa hana mamlaka nayo.
Nao baadhi ya wenyeviti wa serikali za mitaa halmashauri ya mji Kasulu akiwemo mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Kagunga Sara Ndabaharie, Mwenyekiti wa mtaa wa Kagera Helman Mpihigwa na Mwenyekiti wa mtaa wa Muhunga Majuto Mahembe wamesema mafunzo hayo yatawasaidia katika majukumu yao ikiwemo kukemea vitendo vya rushwa na kusimamia vyema miradi ya maendeleo na kutatua changamoto zilizopo katika maeneo yao.