Wananchi washirikishwe utekelezaji wa miradi Kasulu
11 December 2024, 09:42
Katibu tawala Wilaya Kasulu Mkoani Kigoma amewataka viongozi kuhakikisha wanafanya juhudi zote za kuwashirikisha wananchi kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maenedeleo ili kusaidia kutogomea miradi au kuhujumiwa katika maeneo yao.
Na Michael Mpunije – Kasulu
Viongozi wa Serikali za mitaa halmshauri ya mji Kasulu Mkoani Kigoma wametakiwa kuwashirikisha wananchi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuepuka changamoto ya wananchi kugomea miradi hiyo.
Wito huo umetolewa na Katibu tawala Wilaya ya Kasulu Bi, Theresia Mtewele wakati akizungumza na watumishi wa Serikali katika halmshauri hiyo na kuwataka wenyeviti wa mitaa kutoa taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi ili kuongeza chachu ya maendeleo katika mitaa yao.
Bi, Mtewele amesema wenyeviti wa mitaa wanatakiwa kufuata utaratibu wa kufanya mikutano kila baada ya miezi 3 ili kujadili maendeleo ya mitaa hiyo pamoja na kuibua kero za wananchi ziweze kutaftiwa ufumbuzi na kushirikiana kubuni miradi ya maendeleo.
Aidha Bi, mtewele amewataka wenyeviti wa mitaa na watendaji wa kata kuhakikisha wanaimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yao ili shughuli za uzalishaji ziweze kufanyika kwa amani ili kuongeza kipata kwa wananchi.