REA yazindua mradi kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia
5 December 2024, 14:49
Serikali imeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kuhakikisha kilamwananchi anakuwa na uwezo wa kutumia majiko ya gesi ili kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji miti kiholela.
Na Tryphone Odace – Kigoma
Serikali kupitia wakala wa Nishati vijijini REA imetenga shilingi bilioni 8.6 kwa ajili ya mradi wa uuzaji wa majiko ya gesi kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mhandisi mwandamizi wa Miradi kutoka REA Mhandisi Deusdedith Malulu amesema majiko laki nne na nusu yatauzwa kwa wananchi kwa bei ya ruzuku.
Mhandisi Deusdedith amesema mkakati huo unakusudia kuhakikisha huduma za nishati zinafika kila sehemu ambapo pia wameanza kutoa mikopo kwa ajili ujenzi wa vituo vya mafuta maeneo ya vijijini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa Kigoma Kamishna Jenerali wa Jeshi la zimamoto Thobias Andengenye amesema kuwa mpango huo wa matumizi ya nishati safi ya kupikia utawasaidia wananchi na kupunguza uharibifu wa mazingira kwa matumizi ya nishati chafu ya kupikia.