Baiskeli 27 zagawiwa kwa wakulima wawezeshaji wa zao la pamba
3 December 2024, 11:22
Mkuu wa Wilaya Kasulu Mkoani Kigoma Kanali Isac Mwakisu amesema serikali itaendelea kuwasaidia wakulima kwa kuwawezesha nyenzo mbalimbali zitakazowawezesha kulima kilimo chenye tija.
Na Michael Mpunije – Kasulu
Halmshauri ya wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma imekabidhi baiskeli 27 kwa wakulima wawezeshaji wa zao la Pamba ili zitumike kutembelea na kuhamasisha wakulima wa zao hilo kuongeza uzalishaji na kufikia malengo yaliyowekwa na serikali.
Akikabidhi baiskeli hizo mkuu wa Wilaya ya Kasulu kanali Isaac mwakisu amewataka wakulima wawezeshaji na AMCOS mbalimbali zilizokabidhiwa baiskeli hizo zitumike katika kufikia matarajio ya kutoa Elimu kwa wakulima wengi zaidi na kuongeza bidii katika uzalishaji wa zao la Pamba wilayani Kasulu.
Mkaguzi wa Pamba wilaya ya Kasulu Bw.Michael kihiga amesema wanatarajia kufikia malengo ya uzalishaji wa zaidi ya kilo milioni 5 za pamba katika msimu huu wa kilimo licha ya msimu uliopita kushindwa kufikia malengo kutokana na mvua nyingi zilizoathiri uzalishaji wa zao hilo la Biashara.
Kwa upande wake Anna titus mwanandota mkulima mwezeshaji kata ya nyamyusi na na Mariamu James mwenyekiti wa AMCOS mwitiri kata ya Asante Nyerere wamesema baiskeli hizo watazitunza na kuhakikisha wanafikia walengwa wote ili waweze kunufaika na kilimo cha pamba.