DC Uvinza awataka wagombea waliowekewa pingamizi kukata rufaa
14 November 2024, 13:14
Wakati muda uliowekwa kwa wagombea waliowekewa pingamizi ukikaribia kuisha, Mkuu wa Wilaya Uvinza Mkoani Kigoma ametaka wagombea kuwasilisha rufaa zao mapema kabla ya muda wa ziada kuisha.
Na Sofia Cosmas – Uvinza
Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma Dina Mathamani amewataka wagombea katika uchaguzi serikali za mitaa waliowekewa pingamizi kukata rufaa ili kupata haki zao za msingi za kugombea katika nafasi mbalimbali uchaguzi serikali za mtaa utakaofanyika novemba 27 mwaka huu.
Mh. Dina Mathamani ameeleza hayo wakati akizungumza katika kipindi cha Goodmorning Kigoma kinachorushwa na Redio Joy Fm, ambapo amewataka wagombea uchaguzi serikali za mtaa katika wilaya ya uvinza kutumia muda ulioongezwa ili kupata haki yao ya msingi.
Aidha amewataka wananchi kuwa na uelewa ili kupata viongozi wa kijiji ambao watawatetea na kusimamia yale ambayo serikali imepanga kwa mustakabali wa taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Mh. Dina Mathamani amemshukuru Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha ya miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika wilaya hiyo.
Kutokana na miundombinu ya shule kuimarishwa katika wilaya ya uvinza imepelekea ufaulu wa darasa la saba kupanda na kuibuka kididea kwa kushika nafasi ya kwanza kwa miaka miwili mfululizo.