Dkt. Chuachua ahimiza wakulima kulima zao la michikichi Kigoma
5 November 2024, 15:34
Manispaa ya Kigoma Ujiji Mkoani Kigoma imesema itaendelea kugawa miche ya michikichi kwa wakulima ili kuhakikisha inatekeleza agizo la Waziri Mkuu wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa la kila halmashauri kugawa miche kwa wakulima kama mkakati wa kukabiliana na uhaba wa mafuta Nchini.
Na Lucas Hoha – Kigoma
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Rashid Mohamed Chuachua amewataka wananchi kujikita katika kilimo cha zao la michikichi ya kisasa aina TENERA ambayo inachukua muda mfupi kutoa matunda ili kuisaidia nchi kukabiliana na changamoto ya uhaba wa mafuta ya kupikia.
Dkt. Chuachua ameyasema hayo wakati akizundua kitalu cha kuzalishaji miche ya michikichi katika Manispaa ya Kigoma Ujiji zoezi lililoenda sambabmba na kugawa miche ya michikikichi kwa baadhi ya wakulima ambapo amesema zao hilo ni lakimkakati na dhamira ya serikali ni kuhakikisha wakulima wanapatiwa miche hiyo ya kisasa bure.
Awali akitoa taarifa ya hali ya uzalishaji wa miche ya michikichi Afisa Kilimo wa Manispaa ya Kigoma Ujiji ambaye pia ni mratibu wa zao la hilo Paschal Bahati amesema tangu serikali kulitangaza zao la michikichi kuwa lakimkakati Manispaa ya kigoma Ujiji imeshazalisha miche zaidi ya laki 300,000 na kuigawa kwa wakulima.
Kwa upande wao, baadhi ya wakulima ambao wamepatiwa miche ya michikichi wameshukuru serikali kwa kutoa miche hiyo kwani itawasaidia kuzalisha kwa tija tofauti na awali kwani zao hilo ni la muda mfupi, huku wakiomba serikali kuendelea kuzalisha miche hiyo na kuwapatia wakulima ili waondokane na umasikini.
Itakumbukwa kuwa mwaka wa 2018/2019 Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa alitoa maagizo ya kulifanya zao la michikichi kuwa zao la kimkakati na katika maagizo hayo kila Halmashauri iliagizwa kuzalisha miche ya michikichi milioni Moja 1,000,000/ ifikapo June 2025 na kuigawa miche bure kwa wakulima.