Joy FM

Bilioni 20 kutumika ujenzi wa barabara Buhigwe

25 October 2024, 16:11

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya nyongeza kutoka mradi mkuu wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami Kabingo, Kasulu hadi Manyovu yenye urefu wa Km. 260, kukamilisha miradi hiyo kwa wakati ili kuendana na malengo ya serikali sambamba na kuharakisha utoaji huduma kwa jamii.

Na, Josephine Kilavu

Andengenye amesema hayo akiwa  wilayani Buhigwe kwenye ziara yake ya kukagua miradi hiyo inayotekelezwa kwa thamani ya Shilingi Bil. 20 katika wilaya za Buhigwe, Kasulu na Kibondo ikihusisha ujenzi wa Masoko, Stendi, Miundombinu ya Maji, Elimu na uboreshaji wa vituo vya kutolea huduma za Afya.

Mkuu wa mkoa

Amesema wakandarasi hao wanapaswa kuzingatia makubaliano yao na serikali ili  kuhakikisha miradi hiyo ya nyongeza  inakamilika sambamba na ujenzi wa barabara ya  Kabingo hadi Manyovu.

Mkuu wa mkoa

Upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kigoma Mha. Narcis Choma amesema kupitia utaratibu huo,  katika wilaya ya Buhigwe inatekelezwa Miradi ya ujenzi wa Soko la Mnanila, stendi ya mabasi Buhigwe, matanki ya kuhifadhi Maji katika vijiji vya Bweranka na Kibwigwa pamoja na ujenzi wa Shule ya Sekondari Kidato cha Tano na Sita Buhigwe.

Mha. Choma amesema miradi hiyo itakapokamilika wananchi wataona thamani ya ziada ya utekelezaji wa miradi ya barabara katika maeneo yao ikiwemo ujenzi na maboresho ya miundombinu mbalimbali ya kutolea huduma za jamii.