Askofu Bwatta awataka waumini kujiandikisha daftari la kura
15 October 2024, 12:12
Viongozi wa dini wametakiwa kuendelea kuwahamasisha waumini wao kuendelea kujitokeza na kujiandikisha kwenye daftari la mkazi ili waweze kupata nafasi ya kushiriki kwenye uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa.
Na Lucas Hoha – Kasulu
Askofu wa Kanisa la Anglikani Dayosisi ya Western Tanganyika Mhashamu Emmanuel Bwata amewaomba waumini wa Kanisa hilo kujitokeza kujiandisha kwenye daftari la mkazi kwa ajili ya uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa ili kupata viongozi wenye hofu ya Mungu watakaokataa rushwa katika jamii na vitendo vya ukatili kwa wananchi.
Hayo yamejiri katika Ibada maalumu ambayo imefanyika katika kanisa kuu la Anglikani lililopo katika Mji wa Kasulu mkoani Kigoma, iliyolenga kufungua sinodi ya 18 ya kanisa hilo na kuwawekea mikono waumini ambao wamefundishwa mafunzo ya kipaimara
Bwatta ametumia Ibada hiyo kuwakumbusha waumini kutimiza haki ya msingi ya kujiandikisha kwenye daftari la mkazi ili wawe na sifa ya kupiga au kupigiwa kura kwenye uchaguzi utakaofanyika Novemba 27 mwaka huu.
Naye Askofu wa Dayosisi ya Lake Rukwa Efraimu Ntikabuze awali akitoa mafundisho matakatifu amesema kipindi hiki cha uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa na uchaguzi wa serikali kuu mwaka 2025, kuna kila sababu ya kanisa kumuomba Mungu ili amani izidi kudumu katika Taifa la Tanzania.
Nao baadhi wa washirika wa Kanisa hilo wamesema wamepokea hamasa ya Askofu ya kuwataka kujiandisha kwa ajili ya uchaguzi wa viongozi wa serikali za Mitaa, nakuwa watafanya hivo ili kupata viongozi wenye hofu ya Mungu.