Wananchi waomba viongozi kuishi maono ya hayati Mwalimu Nyerere
15 October 2024, 11:45
Mkuu wa Wilaya Kasulu mkoani Kigoma Kanali Isac Mwakisu amesema serikali na viongozi wataendelea kuyaenzi na kusimamia misingi iliyowekwa na mwaasisi wa taifa hili hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Na Lucas Hoha – Kasulu
Wananchi wa kijiji cha Mvugwe kata ya Nyamidaho Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma wamesema watayaenzi na kuyaishi maono ya aliyekuwa Rais wa awamu ya kwanza Tanzania Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ikiwemo kufanya kazi kwa bidii, kupinga rushwa na uonevu kwenye jamii.
Wameyasema hayo kwenye maadhimisho ya miaka 25 ya kifo cha Baba wa Taifa hayati Julius Kambarage Nyerere ambayo kwa wilaya ya Kasulu yamefanyika katika kata ya Nyamidaho yakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Kanali Isaac Mwakisu
Wamesema Baba wa Taifa ni mfano wa kuigwa katika jamii kwani alikuwa ni mwenye upendo na aliyekuwa anapenda kufanya kazi nakuwa wataiga mfano huo kwa kufanya kazi na kuondokana na umasikini.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Isaac Mwakisu pamoja na mambo mengine amesema serikali ya awamu ya sita inaendelea kuyaishi maono ya Baba wa Taifa kwa kuhakikisha ustawi wa jamii unakuwa imara, na serikali imekuwa ikifanya hivyo kwa kuboresha utoaji wa Elimu na uboreshwaji wa utoaji wa huduma za Afya kwa wananchi.
Naye katibu tawala wa Wilaya ya Kasulu Bi Theresia Mtewele amesema wakati wakikumbuka kifo cha hayati Baba wa Taifa, serikali imefanya maboresho makubwa ya mindombinu katika Mkoa wa Kigoma, ikiwemo ujenzi wa barabara, uboreshwaji wa bandari za Ziwa Tanganyika na uboreshwaji wa uwanja wa ndege.
Amesema serikali imeendelea kuhakikisha inaboresha huduma na kusimamia misingi yote iliyoasisiwa na hayati mwalimu nyerere.
Masuala mengine ambayo yamefanyika katika maadhimisho hayo wananchi wamehimizwa kujiandikisha kwenye daftari la mkazi na kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa ifikapo November 27 Mwaka huu.