Viongozi wa siasa, dini Kigoma wakoshwa na maandalizi ya uchaguzi
3 October 2024, 15:09
Viongozi wa dini na vyama vya siasa mkoani kigoma wamesema wameridhishwa na hali ya maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika novemba 27 mwaka huu.
Na Josephine Kiravu – Kigoma
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye amekutana na Viongozi wa Vyama vya Siasa, Dini na watendaji wa Mkoa wa Kigoma kwa lengo la kutoa taarifa kuhusu maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.
Akuzungumza na viongozi hao Mhe. Andengenye amewataka wawakilishi hao kwenda kuwa mabalozi wazuri katika kuhamasisha wananchi kujitokeza katika kujiandikisha kupiga kura au kupigiwa kura ili nchi iweze kupata viongozi bora watakaotokana na maamuzi ya wananchi.
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia Makini Mkoa wa Kigoma Ramadhani Kwezi amesema ameridhishwa na hatua za awali kuelekea uchaguzi huo ikiwemo ushirikishwaji wa vyama vya Siasa katika hatua zote za Maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa.
Kwa upande wake, Upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa (TCD) wilaya ya Kigoma Yassin Bakari amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu kwa kuendelea kuimarisha Demokrasia ikiwemo kutoa fursa sawa kwa vyama vya siasa katika kushiriki michakato ya uchaguzi.
Nao baadhi ya viongozi wa dini waliohudhuria kikao hicho akiwemo Mch Melikizedeki Hoza ambae ni msaidizi wa askofu KKKT pamoja na Kapipi Baraka mjumbe wa baraza la Masheikh BAKWATA wamesema watahakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kuwaeleza wananchi faida za kupiga kura kwa maendeleo ya mkoa na nchi kwa ujumla.
Mkuu wa Mkoa amesema Jumla ya Vijiji 306, vitongoji 1,858 na Mitaa 176 itahusika na uchaguzi huo unaolenga kupatikana kwa wenyeviti wa vijiji, wajumbe wa Halmashauri za vijiji, wenyeviti wa vitongoji, wenyeviti wa Mitaa, wajumbe Kamati za Mitaa huku ukihusisha vituo 2252 vya kupigia kura kimkoa.