Joy FM

Wazee walia na shutuma za ushirikina Kigoma

2 October 2024, 17:41

Baadhi ya wazee wa mkoa wa Kigoma wakiwa katika maadhimisho ya Siku ya Wazee, Picha na tovuti ya mkoa Kigoma

Serikali mkoani Kigoma imesema itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali na mashirika ili kuhakikisha wazee wanasaidiwa na kupata mahitaji yao muhimu ikiwemo kuchukua hatua za kuboresha maisha yao.

Na Kadislaus Ezekiel – Kibondo

Wazee mkoani Kigoma, wameiomba serikali kuingilia kati unyanyasaji wanaofanyiwa wakituhumiwa kujihusisha na viendo vya ushirikina ambavyo vimepelekea baadhi yao kupoteza maisha na wengine kudhoofika kiuchumi na kubaki bila msaada huku jamii ikiwatenga.

Wamesema hayo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wazee Kimkoa, yaliyofanyika kata ya Kitahana wilayani Kibondo ambapo pia wameomba serikali kutatua changamozo zinazowakabili ikiwemo ukosefu wa bima za afya zilizoboreshwa ili kuwa na uhakika wa  kutibiwa  magonjwa mbalimbali.

Ni miongoni mwa wazee waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika wilayani Kibondo, Picha na tovuti ya mkoa
Sauti ya wazee wakiwa katika maadhimisho ya Siku ya Wazee Kibondo

Katika hatua nyingine wazee hao wameomba kutimiziwa mahitaji ya kibinaadamu kulingana na wengi wao kushindwa kumudu gharama za maisha.

Sauti za wazee Kibondo wakiwa kwenye maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani

Akizungumza kwa niaba ya mashirika yasiyo ya kiserikali, Mkuu wa Shirika la Helpage Tanzania wilayani Kibondo Yovitha Mrina, amesema wataendelea kutatua changamoto za wazee, huku Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Kigoma Petro Mbwanji akisema kutokana na umuhimu wa wazee katika taifa wataelimisha jamii kutambua umuhimu wao na watambue haki za wazee.

Sauti ya Mkuu wa Shirika la Helpage Tanzania Yovitha Mrina, Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Kigoma Petro Mbwanji

Katika taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Kanali Agrey Magwaza amesema serikali inaendelea kuchukua hatua kuboresha mahitaji ya wazee.

Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Kanali Agrey Magwaza akizungumza katika maadhimisho ya siku ya wazee duniani, Picha na tovuti Mkoa Kigoma
Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Kanali Agrey Magwaza akizungumza katika maadhimisho ya siku ya wazee duniani.