Joy FM

Shule ya Ndalichako yakabiliwa na upungufu wa madawati

26 September 2024, 12:35

Mwonekano wa shule ya msingi Ndalichako iliyopo Halmashauri ya Mji Kasulu, Picha na Hagai Ruyagila

Serikali imesema itandelea kushirikiana na wadau katika kuboresha miundombinu ya shule ili kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira rafiki.

Na Hagai Ruyagila

Shule ya msingi Ndalichako iliyopo Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa madawati, ukosefu wa huduma ya umeme na ukosefu wa uzio hali inayopelekea kuwa kikwazo katika maendeleo ya kitaaluma kwa wanafunzi.

Hayo yameelezwa na Judith Eliya mwanafunzi wa darasa la saba wakati akisoma risala mbele ya mgeni rasmi Diwani wa kata ya Murusi Fanuel Kisabo katika mahafali ya kwanza ya shule ya msingi Ndalichako.

Amesema shule hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zimekuwa kikwazo katika maendeleo ya kitaaluma shuleni hapo.

Sauti ya Judith Eliya mwanafunzi wa darasa la saba wakati akisoma risala mbele ya mgeni Diwani wa kata ya Murusi Fanuel Kisabo

Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule hiyo Abel Nagana amewasisitiza wanafunzi hao kuzingatia maadili mema waliyojifunza shuleni hapo na kuepukana na masoko ya usiku ambayo si salama katika maisha yao.

Sauti ya mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ndalichako Abel Nagana

Naye Diwani wa kata ya Murusi Fanuel Kisabo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA amesema changamoto zizizopo ni nyingi lakini ametoa shilingi laki moja taslimu na kufanya harambee ambapo imepatikana shilingi laki mbili na elfu hamsini ili kutatua changamoto ya huduma ya umeme katika shule hiyo.

Diwani wa kata ya Murusi Fanuel Kisabo akizungumza katika mahafali ya shule ya Msingi Ndalichako, Picha na Hagai Ruyagila

Pia Kisabo amehidi kuwatengenezea kabati ya kuhifadhia nyaraka za mbali mbali za serikali pamoja na vitabu ili kuvihifadhi katika sehemu salama.

Sauti ya Diwani wa kata ya Murusi Fanuel Kisabo

Shule ya msingi Ndalichako nimiongoni mwa shule tatu zilizoanzishwa mwaka 2023 katika kata ya Murusi kufuatia uwepo wa mrundikano wa wanafunzi kwenye baadhi ya shule za msingi zilizokuwepo ndani ya kata hiyo.