Auwawa na watu wasiojulikana, mwili watupwa korongoni
25 September 2024, 14:03
Wananchi wa mtaa wa Gezaulole Manispaa ya Kigoma Ujiji wameliomba jeshi la polisi kuendelea kufanya doria na kuwadhibiti watu wanaojihusisha na uhalifu kwenye jamii hasa wizi na ukabaji.
Na Josephine Kiravu
Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina maarufu Maneno Bufa mkazi wa Geza Ulole ambaye pia anatajwa kujihusisha na matukio ya uhalifu ameuwawa na watu wasiojulikana huku mwili wake ukitelekezwa eneo la Relini jirani na chanzo cha maji cha Nyakageni Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Unaweza ukadhani upo kwenye sherehe lakini si hivyo hao ni baadhi ya wananchi wa mtaa wa mwenge na maeneo jirani wakishangilia kufuatia tukio la kuuawa kwa Maneno Bufa ambaye wanamtaja kama mhalifu sugu wa ukabaji katika maeneo yao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao wamesema wanatambua ni kosa kuchukua sheria mkononi lakini wamefurahia tukio hilo huku wakilitaka jeshi la polisi kukomesha vitendo vya uhalifu hasa maeneo ya relini kwani vinarudisha nyuma maendeleo yao.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa mtaa wa Mwenge Tatu Haruna Kinga amekiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba mtu huyo amekuwa akihusishwa kwa kiasi kikubwa na matukio ya uhalifu na kuwa hata kifo chake hakijashtua watu wengi.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Kigoma SACP Filemon Makungu amekiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba yupo ziara atakaporejea atatoa taarifa kuhusu tukio hilo lakini tayari askari polisi wamefika eneo hilo na kuchukua mwili wa marehemu kwa ajili ya taratibu zingine.