Serikali yatumia bilioni 19 kuboresha sekta ya afya Kigoma
19 September 2024, 10:39
Serikali imesema kuwa itaendelea kujenga na kuboresha miradi mbalimbali hususani miradi ya afya kwa lengo la kuwaletea maendeleo wananchi na kupata huduma karibu na maeneo yao.
Na James Jovin – Kibondo
Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita serikali imefanya uwekezaji wa Zaidi ya shilingi bilioni 19 katika sekta ya afya kwa mkoa wa Kigoma pekee ikiwa ni mkakati wa kuboresha huduma za afya na kupunguza vifo vitokanavyo na ukosefu wa dawa muhimu na vifaa tiba.
Hayo yamebainishwa na naibu waziri wa wizara ya Tamisemi bi. Zainabu Katimba wakati wa ziara ya naibu waziri mkuu na waziri wa Nishati Dr. Dotto Biteko katika wilaya ya Kibondo.
Aidha mbunge wa jimbo la Muhambwe Dr. Frolence Samizi amesema kuwa wilaya ya Kibondo imefunguliwa katika miundo mbinu mbali mbali hasa ujenzi wa madarasa ya shule za msingi na sekondari hivyo kuinua taaluma kwa kiasi kikubwa.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye ameipongeza serikali kupitia kwa raisi samia kwa kazi kubwa waliyoifanya hasa katika mkoa Kigoma kwa kufungua miundo mbinu ya barabara zilizokuwa tatizo kubwa ndani ya mkoa huo.
Nae naibu waziri mkuu na waziri wa nishati Dotto Biteko amesema kuwa serikali inaendelea kufanya kazi kubwa ya kujenga miundo mbinu na uchumi wa nchi hivyo kila mmoja anapaswa kuunga mkono juhudi za serikali na si kubeza maendeleo yaliyopo.