Mkandarasi atakiwa kukamilisha mradi wa maji kwa wakati
10 September 2024, 08:50
Kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi wilayani Kasulu mkoani Kigoma kimemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji wa miji 28 katika halmashauri hiyo kutekeleza mradi huo kwa wakati ili uanze kutoa maji kwa wananchi.
Na Michael Mpunije – Kasulu
Mkandarasi wa ujenzi wa mradi wa maji wa miji 28 katika halmashauri ya mji wa Kasulu mkoani Kigoma ametakiwa kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi huo kuhakikisha unakamilika kwa wakati ili uweze kutoa huduma kwa wananchi.
Wito huo umetolewa na mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi wilaya ya Kasulu Mberwa abdalla Chibwede alipotembelea katika mradi huo ikiwa ni katika ziara ya kamati ya siasa wilayani Kasulu kukagua miradi ya maendeleo.
Bw. Chidebwe amesema kasi ya ujenzi wa mradi huo ni ndogo ukilinganisha na muda uliopangwa kukamilika kwa ujenzi huo na kwamba mkandarasi anatakiwa kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi huo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa maji safi na usafi wa mazingira wilaya ya Kasulu Kuwasa Mhandisi Gutta Bundala amesema mradi huo unalenga kuwahudumia zaidi ya wananchi laki moja katika halmashauri ya mji wa Kasulu na mpaka sasa ujenzi huo umefikia 33%.
Naye mhandisi wa mamlaka ya maji kasulu, Kuwasa Goodluck Shefatia amesema wameshapokea mabomba ili kuendelea na ujenzi wa mradi huo.
Hata hivyo wajumbe wa kamati ya siasa ya chama cha Mapinduzi wilaya ya Kasulu pamoja na baadhi ya viongozi wa serikali wameomba mkandarasi kuongeza vibarua na mafundi ili kuongeza kasi ya ujenzi na kutoa ajira kwa vijana.