Joy FM

Wenyeviti watakiwa kusimamia usafi wa mazingira Kasulu

27 August 2024, 13:38

Wananchi katika maeneo mbalimbali wakiendelea na usafi wa mazingira katika Halmashauri ya mji wa Kasulu, Picha na Hagai Ruyagila

Wenyeviti wa mitaa katika halmashauri ya mji wa Kasulu mkoani Kigoma wametakiwa kushirikiana na viongozi wa kata kuhamasisha usafi wa mazingira ili kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Katika zoezi la usafi ambalo limefanyika katika mtaa wa Sido kata ya Murubona halmashauri ya mji wa Kasulu limeibua hisia mseto baada ya kuonekana kukithiri kwa uchafu katika mitaro ya kupitisha maji ambayo ipo karibu na makazi ya wananchi.

Mkuu wa kitengo cha usafi wa mazinigira na udhibiti wa taka ngumu halmashauri ya mji wa Kasulu Bw. Msafiri Charles amesema wameweka mikakati ya kuhakikisha usafi wa mazingira katika halmashauri hiyo unaimarika kwa kuwataka wenyeviti wa mitaa kusimamia suala hilo.

Kwa upande wake mwenye kiti wa mtaa wa Sido Bw. Jumanne Mustapha amesema kutokana na kukosekana kwa magari ya kutosha ya kubeba taka imekuwa chanzo cha taka kuendelea kuongezeka.

Diwani  wa kata ya Murubona Bw. Emmanuel Kisunzu amesema mwitikio wa wananchi kufanya usafi bado ni mdogo na kueleza kuwa  kulingana na hali ya usafi ilivyo ipo hatari ya wananchi kupata magonjwa ya mlipuko ikiwa hawatachukua tahadhari mapema.