TALGWU yapongeza serikali kupandisha madaraja watumishi
21 August 2024, 13:05
Wanachama wa chama cha wafanyakazi wa Serikali za mitaa TALGWU mkoa wa kigoma wameomba viongozi wa chama hicho kuendelea kuwasaidia na kuwasemea serikalini ili waweze kupata stahiki na haki zao.
Na James Jovini – Kibondo
Chama cha wafanyakazi wa serikali za mitaa Tanzania TALGWU mkoa wa Kigoma kimeipongeza serikali ya awamu ya sita kwa namna ambavyo imekuwa ikiwajali watumishi kwa kuwapandisha madaraja na kuwapa stahiki zao muhimu hali ambayo inaongeza motisha na uwajibikaji kazini
Hayo yamebainishwa na katibu wa chama hicho mkoa wa Kigoma bw. Jonson Fredrick wakati akizungumza na radio Joy katika ofisi za chama cha TALGWU wilaya ya Kibondo wakati wa kikao kazi cha kuangazia shughuli za chama hicho na namna ya kuwasaidia wafanyakazi kutatua changamoto mbali mbali.
Aidha amesema kuwa chama cha wafanyakazi wa serikali za mitaa Tanzania TALGWU katika mkoa wa Kigoma kimejipambanua kuwasaidia wanachama wake lakini pia kutoa elimu ili waweze kufahamu haki na wajibu kwa masirahi ya jamii na taifa zima.
Kwa upande wake mwenyekiti wa TALGWU mkoa wa Kigoma bw. Yasin Tenganya licha ya shukrani ameitaka serikali kuendelea kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili wafanyakazi hasa walioko katika serikali za mitaa jambo ambalo litaongeza morari kazini na hivyo kuleta maendeleo endelevu.