Shughuli za uvuvi zafunguliwa rasmi ziwa Tanganyika
16 August 2024, 11:09
Serikali imewataka wavuvi wa samaki ndani ya ziwa tanganyika kuacha uvuvi haramu kwa ajili ya uendelevu vsamaki na dagaa.
Na Kadislaus Ezekiel – Kigoma
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amezindua zoezi la uvuvi katika Ziwa Tanganyika baada ya kupumzishwa kwa shughuli za uvuvi katika ziwa hilo kwa muda wa miezi mitatu.
Waziri Ulega amezindua zoezi hilo katika Mwalo wa Katonga manispaa ya Kigoma Ujiji Mkoani Kigoma Agosti 15,2024 na kubainisha kuwa kupumzishwa kwa shughuli za uvuvi kwa miezi mitatu kuanzia Mei 15 hadi Agosti 15 mwaka huu kulikuwa kunalenga kulinda rasilimali za uvuvi kwenye ziwa hilo.
Amesema uamuzi huo wa kupumzisha ziwa ni utekelezaji wa Mkataba wa Kikanda wa Nchi Wanachama wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA) Unaoweka Hatua za Usimamizi wa Uvuvi Endelevu katika Ziwa Tanganyika na Bonde lake.
Aidha, Waziri Ulega ametumia jukwaa hilo kuwaelekeza wavuvi kuwa kufunguliwa kwa shughuli za uvuvi kuendane na matumizi sahihi ya zana na njia halali zinazokubalika kisheria ili samaki walioachwa wazaliane na kuemdelea kupatikana kwa muda mrefu zaidi.
Akizungumza katika zoezi hilo Naibu Katibu Mkuu wizara ya mifugo na Uvuvi, Dk.Edwin Mhede alisema kuwa uvuvi imekuwa moja ya sekta kuu ya uchumi nchini ikiajiri watanzania milioni sita Sawa na asilimia 10 ya Watanzania wote.