Wananchi wamlilia Mchengerwa migogoro ya ardhi
15 August 2024, 08:27
Serikali imesema itaendelea kushirikiana na wananchi ili kubaini na namna ya kutatua migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikisababisha maafa kwa wananchi hususani wafugaji na wakulima nchini.
Na Kadislaus Ezekiel – Kasulu
Wananchi katika kata ya Kagerankanda wilayani Kasulu mkoani Kigoma, wamelalamikia serikali kuchukua ardhi ya kilimo katika eneo la msitu wa akiba makere kusini, kwa kudai eneo hilo walikuwa wakilitumia kwa shughuli za Kilimo, ambapo wamemuomba Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa kusaidia utatuzi wa changamoto hiyo.
Wakiwa katika mkutano na viongozi wa mkoa pamoja na Waziri wa Tamisemi Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, wananchi wamesoma risala ya kijiji na kuomba serikali kurudisha ardhi ambayo wanadai ilichukuliwa bila makubaliano na kukosa sehemu za kilimo.
Hatua hiyo ikamfanya Waziri Mchengerwa kumtaka mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanali Izack Mwakisu kutoa ufafanuzi juu ya suala hilo.
Kisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa akieleza hatua za kuchukua kumaliza mgogoro huo kwa kushirikiana na wizara ya ardhi.