Ukatili unavyowatesa kisaikolojia wanawake Kigoma
14 August 2024, 14:22
Licha ya serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo mkoani Kigoma kuungana na kutoa elimu ya masuala ya ukatilii, bado unyanyasaji wa wanawake kwenye familia umeendelea kuacha simanzi, makovu na huzuni miongoni mwao kwa vipigo ndani ya familia.
Na Ntezimana Gervas – Kigoma
Wanawake mkoani Kigoma wameiomba serikali kuendelea kutoa elimu ya masuala ya ukatili wanaofanyiwa majumbani hasa waliopo kwenye ndoa hususani kipigo ili kuweza kupunguza baadhi ya athari katika ndoa ikiwemo kusambaratika kwa familia.
Wakizungumza na Radio Joy FM, wanawake hao wameeleza kuwa wanapofanyiwa ukatili wanapata athari kubwa zinazosababisha kutofanya shughuli zao jambo linalosababisha kurudi nyuma kiuchumi na kuwaathiri kisaikolojia.
Nao baadhi ya wanaume wameeleza sababu zinazowafanya kutekeleza vitendo vya ukatili ikiwemo baadhi ya wanawake kushindwa kutimiza majukumu yao.
Bw. Rajabu Issa ambaye ni mwakilishi wa Shirika la BACKAIDS, amesema kuwa wanajitahidi kutoa elimu kwa wanawake juu ya kuwaeleza mbinu mbalimbali za kujiepusha na masuala yanayoweza kupelekea kufanyiwa ukatili.
Kwa upande wake, Mkuu wa Dawati la Jinsia manispaa ya Kigoma Ujiji, Jackline Gabriel ameeleza kuwa elimu inaendelea kutolewa katika jamii kuhusu ukatili huku akiitaka jamii kutoa taarifa za vitendo hivyo.