Afukuzwa kazi kwa utoro, kulazimisha kufanya mapenzi na wagonjwa
2 August 2024, 13:39
Baraza la madiwani wilayani Kibondo mkoani Kigoma limemfukuza kazi mtumishi wa idara ya afya, ustawi wa jamii na lishe kwa makosa mbalimbali ikiwemo utovu wa nidhamu.
Na James Jovin – Kibondo
Mtumishi mmoja wa halmashauri ya wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma amefukuzwa kazi baada ya kukutwa na hatia katika makosa ya utoro kazini, ulevi, wizi na kulazimisha kufanya mapenzi na wagonjwa.
Akisoma taarifa ya maamuzi ya baraza la madiwani amemtaja mtumishi huyo kuwa ni Leonard Yusuph Chubwa wa idara ya afya, ustawi wa jamii na lishe.
Aidha amesema kuwa kamati ya fedha, uongozi na mipango iliyofanya kikao tarehe 24/07/2024 ilipokea taarifa iliyokuwa ikihusu kumchukulia hatua za kinidhamu mtumishi Leonard baada ya kupewa onyo mara kadhaa huku akirudia makosa yaleyale na ndipo ukatolewa uamuzi wa kumfukuza kazi.
Uamuzi huo umetolewa baada ya mtumishi ndugu Leonard kupewa onyo na matazamio ya kipindi cha miezi sita kutorudia makosa yanayofanana na hayo lakini alishindwa kufuata maelekezo ya mwajiri wake ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kibondo.