Barabara zawa kero kwa wananchi Mkigo
18 July 2024, 11:39
Wananchi wa vijiji vya kata ya MKigo Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma mkoani Kigoma, wameiomba serikali kutatua changamoto zinazowakabili, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara zilizoharibika kutokana na mvua nyingi zilizonyesha msimu wa mwaka 2023-2024, huduma za umeme wa REA na kuwasogezea huduma ya maji safi na salama karibu.
Na, Kadislaus Ezekiel
Wakiwa katika mkutano ngazi ya kata ulioratibiwa na Chama Cha Mapinduzi, wananchi wametoa kero zao, wakiomba changamoto za miundombinu ya barabara na madaraja kujengwa upya na kutatua kero ya ukosefu wa maji safi na salama.
Wakieleza utatuzi wa kero hizo, Meneja wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini RUWASA Mhandisi Yesaya Elya amesema serikali katika kuwaondolea wananchi adha ya maji, inajenga mradi wa maji mkubwa utakaokidhi mahitaji ya maji kwa wananchi, huku Kaimu Mratibu TASAF Halmashauri ya Kigoma George Vangisauli akitoa maelekezo kuwa kaya masikini kuendelea kufanya kazi za uzalishaji.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi kata ya Mkigo Norbert Nyabakari amepongeza serikali kwa kuendelea kujenga miradi ya maendeleo huku Diwani wa kata ya Mkigo Bakeyemba Jabu akieleza kuwa TANESCO wanaendelea kufanyia kazi tatizo la ukosefu wa umeme kwa wananchi.