Watumishi watakiwa kubuni vyanzo vya mapato kigoma
18 July 2024, 08:38
Serikali mkoani kigoma imewataka watumishi kusimamia ukusanyaji wa mapato ili ksaidia kupata mapato yatayosaidia katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Na Tryphone Odace – Kigoma
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Jenerali mstaafu wa jeshi la zimamoto na uokoaji, Thobias Andengenye amewataka watumishi wa Umma Mkoani hapa kuongeza kasi katika ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato ili kuinua kiwango cha makusanyo ya ndani na kuziwezesha halmashauri na Taasisi za Umma kumudu kujiendesha sambamba na kutekeleza miradi ya Maendeleo.
Mhe. Andengenye ametoa kauli hiyo alipozungumza kwenye kikao kazi kilichowakutanisha wataalam kutoka kwenye Taasisi za Umma na Halmashauri za mkoa, kilicholenga kujadili na kubaini fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo mkoani hapa na kupanga mikakati ya namna bora ya kuzitumia ili kuimarisha ukusanyaji wa mapato.
Amesema mkoani Kigoma vipo vyanzo vingi vya mapato, kinachotakiwa ni ubunifu wa watendaji katika ubainifu wa vyanzo hivyo sambamba na usimamizi madhubuti jambo litakaloimarisha uchumi wa mkoa na nchi kwa ujumla.
Aidha Mhe. Andengenye ametoa wito kwa watumishi wa Umma mkoani humo kudumisha utamaduni wa kutoa huduma bora kwa wananchi jambo litakalowafanya wapokea huduma kuzitangaza vizuri kazi zinazofanywa na serikali kupitia taasisi hizo.
Upande wake katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa amesema lengo la kikao hicho ni kufanya mapitio ya vyanzo vya mapato vya Taasisi za Umma na halmashauri ili kupata mbinu bora za kukusanya mapato kwa tija.
Amesema malengo ya mkoa ni kuhakikisha katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 kila halmashauri inakusanya makusanyo ya ndani ili kufikia malengo ya mkoa.
“Kila Taasisi ikae na kufanya mapitio ya vyanzo vyake vya mapato ili kuona namna bora ya kuongeza makusanyo kwa kipindi cha Mwaka 2024/2025 ambapo malengo ya makusanyo kimkoa katika mamlaka za serikaki za mitaa inatakiwa yafikie kiasi cha Shilingi Bil 20 hadi 25 kwa Mwaka” amesema Rugwa.
Pia amezielekeza taasisi hizo kubainisha vyanzo vipya vya mapato na kuviondoa vile visivyo na tija au vyenye kuleta kero kwa wananchi sambamba na kuandaa mazingira bora kwa ajili ya kuvutia wawekezaji.
Kikao hicho kimehusisha wakuu wa Taasisi za Umma, wakurugenzi watendaji wa halmashauri, wachumi, maafisa biashara pamoja na maafisa mipango miji na mipango kutoka halmashauri nane za mkoa wa Kigoma.