NGO’s zatakiwa kuweka uwazi kwenye miradi
17 July 2024, 13:17
Serikali imesema itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa mashirika yasiyo ya kiserikali ili yaweze kufanya kazi katika mazingira bora.
Na Hagai Ruyagila – Kasulu
Mashirika yasiyo ya kiserikali yametakiwa kuongeza uwazi katika utendaji wao wa kazi ili serikali ijuwe namna wanavyotekeleza miradi yao ya maendeleo katika jamii kuliko kufichaficha.
Hayo yameelezwa na katibu tawala wa wilaya ya Kasulu Bi. Theresia Mtewele wakati akimuwakilisha mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanal Isaac Mwakisu katika kikao cha pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali cha kujadili taarifa za utekelezaji robo ya nne ya mwaka 2023/2024 ndani ya ukumbi wa halmashauri ya Mji Kasulu.
Bi, Mtewele amesema serikali inahitaji kujua mapato yanayoingia na kutoka katika mashirika hayo na namna wanavyotumia fedha hizo na endapo watafanya kazi kwa kuficha haitakuwa jambo zuri.
Kwa upande wake mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu Dkt Semistatus Mashimba ameyasisitiza mashiurika hayo kuongeza nguvu kwenye suala la kilimo huku Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Kasulu Mwl. Vumilia Simbeye akiwaomba kuendelea kufanya kazi kwa pamoja ili kuleta chachu ya maendeleo katika halamashauri zote mbili.
Nao baadhi ya wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali yaliyohudhuria kikao hicho wamesema ni vizuri kufanya kazi zao kwa uwazi huku wakiishirikisha serikali maana mashirika mengine yanaweza kufanya kazi kinyume na sheria na maadili ya kitanzania.
Kikao hiki ni cha pamoja cha mashirika yasiyo ya kiserikali kujadili taarifa za utekelezaji robo ya nne ya mwaka 2023/2024 ndani ya ukumbi wa halmashauri ya Mji Kasulu.