Joy FM

Minara 758 kufikisha mawasiliano nchi nzima

16 July 2024, 11:13

Ni muonekano wa mnara wa mawasiliano katika kijiji cha Kumbanga Kata ya Murungu wilayani Kibondo, Picha na Tryphone Odace

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema imedhamiria kujenga minara ya mawasiliano ili kuhakikisha maeneo mbalimbali nchini yanakuwa na mawasiliano ya uhakika na kuchochea maendeleo Kwa wananchi.

Na Tryphone Odace – Kibondo

Waziri wa habari na  mawasiliano Nchini Tanzania Nape Nnauye amesema kuwa wananchi milioni 8.5 watanufaika na  kuunganishwa kwenye mawasiliano kupitia mpango wa uwekwaji minara 758 Nchi nzima kupitia Mfuko wa mawasiliano kwa wote (UCSAF) ili wananchi hususani wa mipakani waweze kuepukana na usumbufu wa mawasiliano hasa wanapokuwa na dharula za magonjwa.

Waziri Nape amesema hayo mara baada ya kutembelea na kuzindua mnara wa mawasiliano katika kijiji cha kumbanga kata ya Murungu wilayani kibondo Mkoani Kigoma ambapo amewataka wananchi wa kijiji hicho kutumia mnara huko Kwa ajili  maendeleo.

Waziri wa habari na  mawasiliano Nchini Tanzania Nape Nnauye

Amesema Serikali itaendelea kuweka minara maeneo ambayo yalikuwa hayajafikiwa na mawasiliano hasa maeneo ya mipakani ili kuondoa changamoto ya wananchi  kitumia minara ya Nchi nyingine.

Awali Mtendaji Mkuu wa mfuko wa mawasiliano Kwa wote UCSAF,  Bi. Justina Mashiba amesema mfuko huo mpaka sasa wamewasha jumla ya minara 186 na kuwa wataendelea kushirikiana na makampuni ya simu ili kuhakikisha minara inajengwa na kufikisha mawasiliano Kwa wananchi.

Mtendaji Mkuu wa mfuko wa mawasiliano Kwa wote UCSAF,  Bi. Justina Mashiba
Mnara wa mawasiliano ambao umejengwa kumbanga wilayani kibodo, Picha na Tryphone Odace

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa kijiji cha kumbanga wilayani Kibondo wamepongeza hatua ya Serikali kujenga mnara huo Kwani hapo awali walilazimika kupanda juu ya miti na milima kutafuta mawasiliano hali ambayo ilisababisha akina mama wajawazito kushindwa kupata huduma hasa wanapohitaji msaada wa dharula.

Sauti ya wananchi wa vijiji vya Bunyambo na Kumbanga Kibondo