DC Kigoma azitaka NGO’s kuzingatia maadili ya kitanzania
4 July 2024, 10:12
Wakati mashirika yasiyokuwa ya serikali yakiendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kuleta maendeleo kwa wananchi kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo yametakiwa kutokubali kutumia vibaya kwa lengo la kuchafua taswira ya nchi na kuharibu maadili.
Na Josephine Kiravu – Kigoma
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Ndugu. Salum Hamis Kali amewataka Viongozi wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali kufanya kazi Wilayani hapo kwa kuzingatia misingi, uzalendo na maadili ya Kitanzania.
Ameyasema hayo July 03, 2024 Katika Kikao kazi cha Siku Moja kilichofanyikia ukumbi wa Redcross Manispaa ya Kigoma/Ujiji chenye lengo la Mashirika kuwasilisha Mipango kazi kwa Mwaka mpya wa fedha 2024/2025.
Amesema mashirika yasiyo ya Kiserikali ni wadau mhimu wa Maendeleo katika kufanya kazi ni lazima wahakikishe wanalinda jamii ya Kitanzania kwa kupinga vitendo na viashiria visivyoakisi maadili ya kitanzania.
Aidha kiongozi huyo ameyataka mashirika hayo kupinga vitendo vya ukatili kwa Wanawake na Watoto, kuijengea uwezo jamii juu ya utoaji taarifa katika mamlaka zinazohusika na kuwajengea Wananchi uwezo kiuchumi, elimu na katika masuala ya kiafya.
Naye Mratibu wa Mashirika Manispaa ya Kigoma Ujiji Bi. Austina Hwago Amesema Wilaya ya Kigoma ina mashirika yasiyo ya Kiserikali yaliyosajiliwa tisini na nane (98) ambayo yamekuwa yakitekeleza miradi ya Maendeleo katika Sekta ya afya, Uchumi, Kilimo, na uvuvi licha ya baadhi ya Mashirika kutotoa taarifa za utekelezaji wao kwa wakati na kutofuata sera za uwazi na Uwajibikaji.
Naye Mwakilishi wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Kigoma na Mjumbe wa Baraza la Mashirika yasiyo ya Kiserikali Taifa (NACONGO) Ndugu. Alex Luoga amewataka Viongozi wa mashirika hayo kuzingatia kanuni na miongozo kwa kutoa taarifa kwa wakati na kuzingatia misingi na maadili ya Taifa.