Madiwani wamtaka DED Kasulu kutoa taarifa ya mapato
2 July 2024, 11:29
Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji Kasulu ametakiwa kutoa taarifa ya mapato ya soko la Kigondo ili kufahamu mapato yanapatikana kwenye soko hilo kama sehemu ya chanzo cha mapato ya halmashauri hiyo.
Na Hagai Ruyagila – Kasulu
Baraza la Madiwani katika halmshauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma limemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kutoa taarifa ya makusanyo mapato kuanzia mwezi aprili hadi mwezi juni mwaka huu kutoka soko la mnadani lililopo kata ya Kigondo ili kubaini upatikanaji wa mapato katika soko hilo.
Akizungumza kwa niaba ya madiwani mwenyekiti wa halmashauri ya mji kasulu bw. Noel Hanura ametoa maagizo hayo baada ya kuona hakuna taarifa ya makusanyo ya mapato kutoka katika soko la mnadani
Bw. Hanura amesema lengo ni kuona makusanyo ya halmashauri yanaongezeka ili kufanikisha mpango wa serikali katika ukusanyaji wa mapato ndani ya halmashauri hiyo.
Kwa upande wake mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Kasulu. Vumilia Simbeye amesema amepokea maagizo hayo na tayari ameshaanza kuyafanyia kazi.
Licha ya Simbeye kuwashukuru wafanyabiashara kwa namna wanavyolipa kodi ya serikali amesema ukusanyaji wa mapato katika halmashauri ya Mji Kasulu unaendelea vizuri na tayari wameshavuka lengo walilojiwekea katika mwaka wa fedha 2023/2024.
Soko la Mnadani ni miongoni mwa masoko makubwa yanayopatika katika halmashauri ya Mji Kasulu.