Wananchi Mwilamvya wachanga milioni 14 kujenga shule mpya
2 July 2024, 08:42
Ili kukabiliana na chamgamoto ya watoto kutembea umbali mrefu kwa wananchi wa kata ya Mwilamvya wilayani Kasulu, hatimaye wananchi wamekubaliana kushirikiana na wadau wa maendeleo kuchanga pesa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa shule mpya katani hapo.
Na Emmanuel Kamangu – Kasulu
Zaidi ya shilingi milioni 14 zimechangwa na wananchi pamoja na wadau wa maendeleo kata ya Mwilamvya halmashauri ya mji wa kasulu ili kufidia eneo ambalo ni mashamba ya wananchi kwa ajili ya kupisha ujenzi mpya wa shule ya msingi Mwilamvya.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara Diwani wa kata ya Mwilamvya halmashauri ya mji wa Kasulu Bw. Emmanuel Gamuye ameendelea kuwaomba wananchi kuchangia michango ili kufanikiwa kufidia eneo husika ambalo limependekezwa kujengwa kwa shule mpya ya msingi ikiwa ni kuwanusuru wanafunzi na adha ya kutembelea umbali mrefu kufuata elimu.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti halmashauri ya mji wa Kasulu Bw. Seleman Kwirusha amewasihi wananchi wa kata ya Mwilamvya kuchangamkia fursa hiyo ili kuharakisha maendeleo hasa kwa kuwasaidia watoto wadogo kupata huduma ya elimu karibu.
Aidha wananchi wa kata ya Mwilamvya wakiwa katika mkutano huo wamesema watahakikisha kwa kila namna wanamuunga mkono Diwani Gamuye ili kufika mwakani shule mpya ya msingi Mwilamvya iwe tayari imekamilika.
Hata hivyo wananchi hao wameongeza kuwa kwa mwananchi atakayekaidi kuchangia mchango wa kuanzia elfu tano kama walivyokubaliana kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya msingi watamuona kama adui namba moja wa maendeleo ya kata yao.